Watu wanne wameuwawa na wengine 20 wamejeruhiwa kwenye mashambulizi ya kupanga ya mabomu na bunduki yaliyomlenga waziri wa ulinzi na wabunge kadhaa katika mji mkuu wa Afghanistan Kabul. Bomu la kwanza lililipuka katikati mwa Kabul Jumanne jioni na kusababisha moshi mzito kutanda katika anga la mji huo. Waziri wa ulinzi Bismillah Mohammadi amesema lilikuwa shambulizi la bomu la kutegwa kwenye gari lililofanywa na mshambuliaji wa kujitoa muhanga lililoilenga nyumba yake na baadhi ya walinzi wake walijeruhiwa. Kabla muda wa masaa mawili kupita, mlipuko mwingine ulifuatiwa na milipuko midogo na milio ya risasi iliyoutikisa mji wa Kabul karibu na eneo lenye ulinzi mkali la Green Zone, ambako ni makazi ya balozi kadhaa ukiwemo ubalozi wa Marekani. Hakuna kundi lililodai kuhusika na hujuma hiyo lakini Marekani inalinyoshea kidole cha lawama kundi la Taliban.


0 Comments